Breaking News

Rekodi Zinavyoibeba Yanga Sc, Ibenge Ajawa Hofu na Baridi Kali

Rekodi Zinavyoibeba Yanga Sc, Ibenge Ajawa Hofu na Baridi Kali

AL Hilal   tayari wapo Dar es Salaam  kuwavaa Yanga katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya makundi, huku kocha wa timu hiyo, Florent Ibenge akiwa na rekodi isiyovutia Benjamin Mkapa.

Al Hilal imepangwa kundi ‘A’  na Yanga ya Tanzania, TP Mazembe ya DR Congo iliyochukua taji la mashindano hayo mara tano na MC Alger kutokea Algeria.

Yanga chini ya kocha mkuu mpya raia wa Ujerumani, Sead Ramovic aliyechukua nafasi ya Miguel Gamondi, rekodi zinaonyesha Ibenge amekuwa na kipindi kigumu na baadhi ya timu mbalimbali alizoziongoza kwenye michuano ya CAF akiwa kwa Mkapa. Ibenge alitua nchini msimu wa 2018-2019, wakati huo akiwa na kikosi cha AS Vita Club ya kwao DR Congo ambacho kilipangwa kundi moja la ‘D’ na Simba, ambapo alijikuta akipoteza baada ya kuchapwa kwa mabao 2-1, mechi iliyopigwa Machi 16, 2019.

Katika kundi hilo la ‘D’, Al Ahly kutoka Misri iliongoza na pointi 10, ikifuatiwa na Simba iliyoshika ya pili na pointi tisa, huku JS Saoura ya Algeria ikishika ya tatu na pointi nane, wakati AS Vita Club iliburuza mkiani na pointi saba.

Msimu huo unakumbukwa zaidi kwa mashabiki wa Simba kwani ilifika hadi robo fainali na kutolewa na TP Mazembe ya DR Congo kwa jumla ya mabao 4-1, baada ya mchezo wa kwanza jijini Dar es Salaam kutoka suluhu kisha ugenini kuchapwa mabao 4-1.

Kocha huyo akatua tena nchini katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu wa 2020-2021 akiwa tena na kikosi hicho cha AS Vita Club ambacho kilipangwa kundi ‘A’ na Simba na kushuhudia akipoteza kwa kufungwa mabao 4-1, Aprili 3, 2021.

Msimu huo Simba iliongoza kundi na pointi 13, nyuma ya Al Ahly ya Misri iliyoshika nafasi ya pili na pointi 11, huku AS Vita Club ikiwa ya tatu na pointi saba wakati Al Merrikh ya Sudan iliburuza mkiani baada ya kukusanya pointi zake mbili.

Msimu huo pia Simba iliishia hatua ya robo fainali baada ya kuondolewa na Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini kwa jumla ya mabao 4-3, baada ya mchezo wa kwanza kuchapwa ugenini mabao 4-0, kisha kushinda Uwanja wa Benjamin Mkapa kwa mabao 3-0.


Baada ya hapo Ibenge akarejea tena Tanzania msimu wa 2021-2022 wakati huo akiwa na kikosi cha RS Berkane kutoka Morocco ambacho kilikuwa Kombe la Shirikisho Barani Afrika kikiwa kundi ‘D’ ambapo alifungwa na Simba bao 1-0, Machi 13, 2022.

Msimu huo, RS Berkane iliongoza kundi na pointi 10 sawa na Simba pia iliyokuwa na pointi 10, huku ASEC Mimosas ya Ivory Coast ikiwa ya tatu na pointi tisa wakati Union Sportive de la Gendarmerie Nationale ya Niger ikiburuza mkiani na pointi tano.

Msimu huo Simba iliishia hatua ya robo fainali baada ya kuondolewa na Orlando Pirates ya Afrika Kusini kwa penalti 4-3, baada ya kikosi hicho cha Msimbazi kushinda mchezo wa kwanza Benjamin Mkapa kwa bao 1-0, kisha ugenini kuchapwa pia 1-0.

Kwa upande wa Yanga rekodi zinaonyesha timu hiyo katika uwanja wa nyumbani kwenye michuano ya CAF kuanzia msimu wa 2022-2023 na 2023-2024, imepoteza mchezo mmoja tu ambao ulikuwa wa fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya USM Alger ya Algeria.

Katika msimu huo wa 2022-2023, Yanga ilipangwa kundi ‘D’ ambapo ilivuna pointi sita nyumbani ikizifunga TP Mazembe ya DR Congo mabao 3-1, 2-0, Real Bamako ya Mali na 2-0, dhidi ya US Monastir ya Tunisia na kuongoza kundi hilo na pointi 13. Pointi hizo zilikuwa sawa na za US Monastir ila Yanga ilikuwa na faida zaidi katika matokeo ya wao kwa wao huku Real Bamako ikimaliza nafasi ya tatu na pointi zake tano, wakati TP Mazembe ya DR Congo iliburuza mkia na pointi tatu tu.

Baada ya hapo Yanga ikatinga robo fainali na ikakutana na Rivers United ya Nigeria ambapo mchezo wa kwanza ikiwa ugenini ilishinda 2-0, huku mechi ya marudiano jijini Dar es Salaam ikatoka suluhu na kufuzu nusu fainali kwa jumla ya mabao 2-0.

Ushindi huo wa jumla ukaipa nafasi Yanga kukutana na Marumo Gallants ya Afrika Kusini ambapo mechi ya kwanza jijini Dar es Salaam ilishinda mabao 2-0, huku marudiano ugenini ikashinda 2-1 na kufuzu fainali kwa mara ya kwanza katika historia yake.

Katika mchezo wa fainali Yanga ikakutana na USM Alger ya Algeria ambapo mechi ya kwanza jijini Dar es Salaam ilichapwa 2-1, huku mechi ya marudiano ikashinda bao 1-0 na kukosa ubingwa kwa faida ya bao la ugenini.

Msimu uliopita ambao Yanga ilikuwa Ligi ya Mabingwa Afrika haikupoteza mchezo wowote nyumbani ambapo ilipangwa kundi ‘D’ dhidi ya Al Ahly kutoka Misri, CR Belouizdad ya Algeria na Medeama SC ya Ghana. Katika kundi hilo Yanga ilivuna pointi saba nyumbani kati ya tisa. Pointi hizo za Yanga zilikuwa sawa na CR Belouizdad ingawa kikosi hicho cha mitaa ya Twiga na Jangwani kilikuwa na faida nzuri zilipokutana huku Al Ahly ikiongoza kundi hilo na pointi 12, wakati Medeama SC iliburuza mkia na pointi zake nne.

Katika hatua ya nusu fainali Yanga ikakutana na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini ambapo mechi ya kwanza jijini Dar es Salaam zilitoka suluhu kama ilivyokuwa pia ugenini na kisha safari yao kuishia hapo baada ya kutolewa kwa penalti 3-2.

Akizungumzia rekodi hizo, Ibenge alisema hawezi kuangalia zaidi michezo iliyopita ingawa anaiheshimu Yanga kwa sababu ni timu iliyobadilika kutokana na ubora wa wachezaji ilionao hivyo, anatarajia kuona mchezo mgumu sana na wenye ushindani.

“Yanga ya sasa na tuliyokutana nayo mara ya mwisho ni vitu viwili tofauti kwa sababu imebadilika kiuchezaji na inajua namna mashabiki na viongozi wao wanataka kutokana na malengo yao, itakuwa mechi nzuri na ya kusisimua kwa pande zote.”

Yanga itaanza kampeni zake katika hatua hiyo ya makundi kwa kucheza na Al Hilal Novemba 26, mwaka huu kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, huku ukiwa ni mchezo wa kisasi kwani mabingwa hao wa Tanzania walitolewa na Wasudani hao msimu wa 2022-2023.

Katika msimu huo wa 2022-2023, timu hizo zilikutana katika hatua ya mtoano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kusaka tiketi ya kutinga makundi ambapo mechi ya kwanza iliyopigwa Benjamin Mkapa Oktoba 8, 2022 Yanga ilitoka sare ya kufungana bao 1-1.

Mchezo wa marudiano uliopigwa Oktoba 16, 2022, kwenye Uwanja wa Al-Hilal jijini Omdurman Sudan, Yanga ikachapwa bao 1-0, lililofungwa na Mohamed Abdelrahman na kutolewa kwa jumla ya mabao 2-1, kisha kuangukia Kombe la Shirikisho na kufika fainali.


Msimu huo ambao Yanga ilifika fainali ilicheza na USM Alger ya Algeria ambapo mechi ya kwanza Dar es Salaam ilipoteza kwa mabao 2-1, Mei 28, 2023, kisha marudiano ikashinda 1-0, Juni 3, 2023 na kukosa ubingwa kwa faida ya bao la ugenini.

Yanga imetinga makundi ya michuano hiyo kwa mara ya pili mfululizo kwa rekodi ya aina yake baada ya kufuzu kwa jumla ya mabao 17, kwani katika mechi zake za raundi ya awali iliiondosha Vitalo kutoka Burundi kwa jumla ya mabao 10-0. Ikakutana na CBE SA ya Ethiopia ambapo mechi yake ya kwanza ugenini ilishinda bao 1-0, marudiano Zanzibar ikashinda mabao 6-0. Al Hilal ilianzia pia hatua za awali iliiondosha Al Ahly Benghazi ya Libya kwa mabao 2-1, kisha raundi ya kwanza ikaitoa San Pedro ya Ivory Coast kwa jumla ya mabao 3-2.

Mchezo huu, hautokuwa rahisi kwa Yanga kwani Al Hilal ina rekodi nzuri kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika ambapo imecheza fainali mbili za mwaka 1987 na 1992, huku ikifika pia nusu fainali mara tano kuanzia mwaka 1966, 2007, 2009, 2011 na 2015.

Pia imecheza robo fainali mbili ya mwaka 1988 na 1990 na kushiriki hatua ya makundi mara nane ikianza mwaka 2008, 2014, 2017, 2019-2020, 2020-2021, 2021-2022, 2022-2023 na 2024-2025 huku Yanga ikitinga makundi mara tatu 1998, 2023-2024 na 2024-2025.

Yanga iliyocheza michezo 10, imeshinda minane na kupoteza miwili ikiwa nafasi ya pili na pointi 24, nyuma ya watani zao wa jadi Simba inayoongoza na pointi 25, ambapo kikosi hicho cha Jangwani kimefunga jumla ya mabao 14 na kuruhusu manne.

Al Hilal ambayo itaanza kucheza na Yanga mchezo wa kwanza wa kundi hilo, inaongoza Ligi ya Mauritania ambapo inashiriki kutokana na machafuko ya kisiasa yaliyopo Sudan, imecheza michezo saba ambapo imeshinda mitano na kutoka sare miwili tu.  Katika michezo hiyo, Al Hilal imekusanya pointi zake 17 ikiwa kileleni mwa msimamo baada ya kufunga mabao 15 na kuruhusu mawili.

No comments